Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNSOM azungumzia kuondolewa kwa Waziri Mkuu Somalia

Mkuu wa UNSOM azungumzia kuondolewa kwa Waziri Mkuu Somalia

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Kay amezungumzia vile ambavyo wabunge wa bunge la nchi hiyo na spika wake walivyoendesha kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu wa nchi hiyo Abdi Farah Shirdon.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, Bwana Kay pamoja na kutoa shukrani kwa Bwana  Shirdon amesema upigaji kura huo wa Jumatatu ambao haukutarajiwa umefanyika kwa mujibu wa katiba ya nchi na kanuni za bunge.

Amesema taasisi nchini Somalia ndio zinakomaa na kwamba Umoja wa Mataifa upo kwa ajili ya kusaidia maeneleo na ujenzi thabiti wa nchi hiyo na ana matarajio ya kushirikiana vyema na mamlaka zitakazochaguliwa. Bwana Kay amesema Shirdon alijitahidi kuendeleza ukuaji na maendeleo na alikuwa mstari wa mbele kujenga mahusiano kati ya wabia wa kimataifa naSomalia.

Ameongeza kuwa jambo muhimu sasa ni kuteua Waziri Mkuu mapema iwezekanavyo ili kuendeleza kasi ya kisiasa na ujenzi wa nchi huku akisema ni matumaini yake kuwa Rais atafanya mashauriano ya kina kabla ya uteuzi.