Mratibu wa UM Afghanistan asikitishwa na vifo vya wafanyakazi wa misaada

2 Disemba 2013

Mark Bowden, mratibu wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya Afghanistan ameelezea huzuni yake kufuatia vifo vya wafanyakazi 9 wa misaada wa Afghanistan katika mashambulio mawili tofauti siku za karibuni. Amesema hadi kufikia sasa mwaka huu pekee Umoja wa Mataifa umerekodi visa 237 dhidi ya wafanyakazi wa misaada, majengo na vifaa vya wafanyakazi hao.

Katika visa hivyo wafanyakazi 36 wameuawa, 24 kuwekwa rumande, 46 kujeruhiwa na wengine 72 kutekwa. Bwana Boweden amesema anatiwa hofu na tabia hiyo katika wakati ambao nchi ya Afghanistan iko katika kipindi kigumu cha mpito ambacho huenda kikasababisha mahitaji zaidi ya kibinadamu.

Ametoa wito kwa pande zote kuheshimu na kutoegemea upande wowote kwa masuala ya wafanyakazi wa misaada, na pia kuheshimu sheria za kimataifa zinazohusu misaada ya kibinadamu.