Huduma za kibinadamu zatangulizwa wakati Ufilipino ikijikwamua kutoka kimbunga Haiyan: UM

2 Disemba 2013

Kufikisha huduma za kibinadamu kwa manusura wa kimbunga Haiyan bado ni suala la kipaumbele kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa na wadau wake, amesema Bwana Haoliang Xu, Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Mpango wa Maendeleo katika Umoja wa Mataifa, UNDP kwenye eneo la Asia na Pasifiki, ambaye pia ni Msimamizi wa Ofisi ya kikanda ya Umoja wa Mataifa kwa ukanda huo.

Akihutubia mkutano wa waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Bwana Xu amesema  hadi sasa, watu milioni 3 wameweza kufikishiwa msaada wa chakula, zaidi ya familia 10,000 zimepokea vifaa vya makazi, na watoto 60,000 kupewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kupooza na surua, na dawa za kuongeza vitamin A.

Ameongeza kuwa kinachozingatiwa sasa ni harakati za kujuikwamua tena.

“Lengo la harakati za kujikwamua ni kuwasaidia watu kurudia maisha ya kawaida, kwa kuwarejesha watoto shuleni, kuwafungulia wanaume kwa wanawake nafasi za ajira, kufungua tena hospitali na kuanzisha tena utoaji wa huduma za umma. Hii ndiyo barabara ya kujikwamua tena, na itasaidia kujenga tena jamii zenye kuweza kuhimili vimbunga kama hivi.”

UNDP na wadau wengine wameanzisha programu za kukarabati na kukwamua maeneo yaloathiriwa, ukiwemo mpango wa utoaji hela kwa watu wanaofanya kazi. Pia amezungumzia mipango ya siku zijazo

“Tukitazama mbele, tutaendelea kufanya kazi na wadau, mashirika ya kijamii na sekta ya kibinafsi, kwa uongozi wa serikali, na kujenga jamii thabiti zaidi na zenye uhimili zaidi. Hivi vitahusisha kuweka mifumo ya kutoa tahadhari mapema, kuwafundisha watoto kuhusu kujiandaa kwa majanga, kuweka makazi ya kuwahamishia watu kwa dharura, kujenga miti inayotoa kinga, kusaidia biashara ndogondogo na kufikisha nishati mbadala kwa jamii za vijijini. Barabara ya kujikwamua ni lazima pia iwe njia ya uendelevu.”