Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumwa nchini Ghana bado unatesa watoto: Mtaalamu

Utumwa nchini Ghana bado unatesa watoto: Mtaalamu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu vitendo vya utumwa vinavyofanyika sasa duniani, Gulnara Shahinian ameitaka serikali ya Ghana kuimarisha hatua zake za kukabiliana na vitendo vya utumwa nchini humo.

Bi. Shahinian amesema hayo leo ambapo dunia inaadhimisha siku ya kutokomeza aina zote za utumwa akieleza bayana kuwa nchiniGhana, utumwa bado uko dhahiri hata kwa watoto walio na umri wa miaka minne na kuendelea.

Amesema ziara ya siku tisa nchini humo imemwezesha kushuhudia watoto wa umri huo wakitumikishwa kwenye vijiji vya jamii za uvuvi ambako wanafanya kazi hatarishi bila malipo huku wakinyimwa hakiyaoya msingi ya elimu.

Halikadhalika alikutana na watoto wa kike wanaojiuza kwenye barabara za mji mkuuAccrana wale wanaolala kwenye mazingira dhalili ya masoko ambao walimweleza mazingira hatarishi  ya kubakwa wanayokumbana nayo.

Mtaalamu huyo ametambua na kusifu hatua za serikali za kupitisha sheria kuondoka na utumwa miongoni mwa jamii lakini amesema bado yahitajika kuhakikisha mipango hiyo inatumika kuleta mabadiliko badala ya kubakia kwenye makabrasha.

Bi. Shahinian ameshauri hatua madhubuti katika kushughulikia chanzo cha utumwa nchini humo ikiwemo umaskini wa kupindukia na tofauti za maendeleo kimaeneo. Ripoti ya ziara yake ataiwasilisha kwenye kikao cha baraza la haki za binadamu mwezi Septemba mwakani.