Uongozi wa Syria wahusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu:Pillay akinukuu ripoti

2 Disemba 2013

Uongozi wa ngazi ya juu wa Syria unahusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliotekelezwa  wakati wa machafuko yanayoendelea nchini humo amesema mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay akinukuu ripoti ya uchunguzi. Assumpta Massoi na ripoti kamili

(RIPOTI YA ASSUMPTA MASSOI)

Akizungumza mjini Geneva Bi Pillay amesema ripoti za tume ya uchunguzi wa ukiukwaji wa haki nchini Syria zinaonyesha kwamba uongozi wa juu wa serikali akiwemo mkuu wa nchi wanaweza kuhusishwa na uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Bi Pillay  hata hivyo amesema orodha ya washukiwa wa uhalifu wa vita aliyokabidhiwa na tume ya uchunguzi ya Syria bado imefungwa hadi pale itakapoombwa na mchakato wa kisheria wa serikali au wa kimataifa.

(Sauti ya Pillay)

Sijasema kuwa mkuu wa nchi ni mshukiwa, bali nilikuwa nanukuu ripoti ya jopo la uchunguzi ambalo lilisema kuwa kwa kuzingatia taarifa zao, uwajibikaji unaelekezwa kwa mamlaka za juu. Uwajibikaji unapaswa kuwa kipaumbele muhimu kwa jamii ya kimataifa na nataka kusema hilo tena na tena wakati mkutano wa pili wa Geneva unapoanza.”

Pillay amezitaka pande zote zinazohusika na mgogoro waSyriakukomesha machafuko na kutoa fursa ya mchakato wa amani unaotarajiwa kuanza Januari mwakani.