Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila hatua madhubuti, tembo wa Afrika kutoweka muongo ujao

Bila hatua madhubuti, tembo wa Afrika kutoweka muongo ujao

Nchini Botswana kunafanyika mkutano wa kubaini mustakhbali wa tembo wa Afrika ambao maisha yao yako mashakani kila uchao kutokana an vitendo vya kijangili. Mkutano huo uliotishwa na serikali ya Botswana kwa ushirika na shirika la kimataifa la uhifadhi wa maliasili, unafanyika wakati takwimu mpya zikisema kuwa bila hatua madhubiti, tembo hao baada muongo ujao watabakia historia. Jason Nyakundi na ripoti kamili.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Kulingana na tathmini mpya kuhusu uwindaji haramu makadirio yanaonyesha kuwa mwaka 2012 ndovu  15,000 waliuawa kwenye maeneo 42 katika  nchi 27 barani Afrika zinazoshiriki kwenye mpango wa kuchunguza uwindaji haramu wa ndovu MIKE.

Kulinga na mpango wa MIKE ndovu 22,000 waliuawa kiharamu kote barani Afrika mwaka 2012 ikiwa ni idadi ya chini kidogo ikilinganishwa na ndovu 25,000 waliouawa mwaka 2011.

Tangu mwaka 2000 hadi 2013 usafirshaji wa pembe za ndovu umeongezeka sawia na kuongezeka kwa biashara ya bidhaa hizo.  Biashara ya pembe za ndovu iliongezeka kwa asilimia 20 kutoka kwa ile iliyoandikishwa mwaka 2011.

Kuanzia mwaka 2009 njia za biashara kwenye bandari za magharibi na kati kati mwa bara la Afrika zilihamia kwenye bandari za mashariki mwa Afrika huku Kenya na Tanzania zikiwa vituo kunakopitishwa  pembe zinazotoka kwenye bara la Afrika. Kiasi kikubwa cha pemba hizi husafirishwa hadi nchini China na Thailand.