Virusi vya MERS Corona vyabainika kwa ngamia Qatar:WHO

29 Novemba 2013

Shirika la afya duniani WHO litatoa ripoti ya uchunguzi kutoka Qatar inayoashiria kuwepo kwa virusi vya MERS Corona miongoni mwa ngamia. Shirika hilo linasema hii ni mara ya kwanza ngamia kuambukizwa virusi vya corona nchini humo lakini njia ya kuambukizwa kwao bado ni kitendawili.

Matokeo ya utafiti huo kwa mujibu wa WHO yanatoa mwangaza wa wapi pa kuangalia na kwa kiasi gani kuna maambukizi hayo miongoni mwa ngamia. Kufuatia hali hiyo watu wanasemekana kuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa hata wale ambao wana magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama kisukari na moyo wametakiwa kukaa mbali na wanyama hao.Glen Thomas ni msemaji wa WHO.

(SAUTI YA GLEN THOMAS)

"Kuna tafiti zaidi zinaendela katika maabara  zote nchini Uholanzi  ambazo zinafanya kazi kwa karibu na Qatar katika uchunguzi huu, kwahiyo hizi ni hatua za mwanzo lakini zenye matokeo ya kusisimua, pia ni mapema kutoa mapendekezo kutokana na tafiti hizi, hata hivyo kuliongana na taswira ya ugonjwa kama tulivyoona katika baadhi ya visa mwaka jana, ni vyema kupendekeza  watu walioko katika hatari ya kuathirika ambao ni watu wenye hali maalum kama wenye magonjwa sugu, wagonjwa wa kisukari, moyo na kadhalika  kuepuka kuwa karibu na wanyama wakiwa wanatembelea mashamba katika ukanda huu."

Utafiti huo unathibitisha kwamba virusi vya MERS corona pia vipo kwa wanyama kama ngamia lakini hakuna uthibitisho wa kuwaambukiza binadamu, au wa jinsi gani virusi hivyo viliwapata wanyama.