Baraza la usalama lalaani vikali shambulio dhidi ya ubalozi wa Urusi Damascus:

29 Novemba 2013

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamesikitishwa na kulaani vikali shambulio la magruneti dhidi ya ubalozi wa Urusi mjini Damascus Syria siku ya Alhamisi. Shambulio hilo limekatili maisha ya mtu mmoja na kujeruhi wengine 9 wakiwemo walinzi wa ubalozi huo.

Wajumbe hao wametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulio hilo ambalo wameliita kitendo cha kigaidi. Wamesema ugaidi wa aina yoyote ile ni moja ya vitisho vikubwa vya amani na usalama na ni uhalifu usiokubalika bila kujali sababu ya kuutekeleza, popote na kwa njia yoyote ile.

Wajumbe hao wamesisitiza haja ya kukabili mifumo yote ya ugaidi kwa kuzingatia mikataba ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na hususani haki za binadamu, tisho la kimataifa, amani na usalama. Wameongeza kuwa ni muhimu wahusika wa vitendo hivyo kufikishwa kwenye mkono wa sheria.