Twaunga mkono mchakato wa kisiasa Yemen, pande ziharakishe ukamilike: Baraza

28 Novemba 2013

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wametoa ujumbe wa pamoja na ulio dhahiri ambao unaunga mkono mchakato wa kisiasa unaoendelea nchini Yemen pamoja na jitihada za serikali ya nchi hiyo za kujenga upya uchumi, kuimarisha usalama ikiwemo mjadala wa kitaifa.

Msimamo huo umeelezwa kwa waandishi wa habari na Rais wa Baraza hilo Balozi Liu Jieyi wa China mara baada ya mashauriano yaliyofanyika kwenye baraza la usalama kuhusu Yemen. Mchakato wa kisiasa unaozungumziwa ulizinduliwa mwezi Machi mwaka huu na unajumuisha kwenye mchakato washiriki wapya wakiwemo vijana, wanawake, wawakilishi wa vikundi vya kiraia pamoja na kikundi cha Houthi na kile cha Hiraak kusini.

Awali mkutano huo wa mjadala wa kitaifa ulipaswa kumalizika tarehe 18 Septemba lakini  kutokuelewana katika masuala muhimu kulisababisha mkutano huo uchelewe kuhitimishwa.

Balozi Liu amesema kutokana na kuchelewa kuhitimishwa kwa mjadala huo, wajumbe wa baraza wameonyesha wasiwasi na kuzitaka pande zote nchini Yemen kushiriki kwa dhati kwa minajili ya kuridhiana na hatimaye kukubaliana masuala ya msingi.

Hofu ya wajumbe hao juu ya hatma ya mchakato huo ni kuwepo kwa ripoti ya baadhi ya watu kuingilia kati kwa lengo la kuupeleka mrama na hivyo wameshutumu hatua zozote za namna hiyo na kuonya kuwa wanaofanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua iwapo wataendelea na tabia hizo.

Kuhusu ongezeko la wito kwa wakazi wa Kusini mwa nchi hiyo kutaka kujitenga, wajumbe wa baraza la usalama wamesema kwa kauli moja kuwa wanaunga mkono umoja, mshikamano, uhuru na mamlaka ya taifa zima la Yemen.