Ban asikitishwa na kusambaa kwa ghasia Misri

27 Novemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anasikitishwa na hatua ya kuwekwa vizuizini, na kusambaa kwa ghasia za waandamanaji nchini Misri ikiwamo taarifa za mashambulio ya kijinsia.

Katika taarifa yake iliyotolewa mjini New York Bwana Ban amesisitiza umuhimu wa kuheshimu maaandamano ya amani na uhuru wa kukusanyika ikiwa ni pamoja na mazungumzo na kuepuka ghasia

Amesema kwa kuwa serikali ya Misri imeridhia sheria ya kuongoza maandamano, ni muhimu kuhakikisha kila sheria ikitekelezwa ithibitishwe na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Ban kadhalika amesisitiza wasiwasi ulioelezwa na kamishina mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa kwamba sheria mpya zilizopitishwa zingeweza kusababisha uvunjaji mkuu wa haki ya uhuru wa kukusanyika kwa amani. Amezitaka mamlaka nchini Misri kuzingatia marekebisho ya sheria, akisema pale kwenye uhuru wa kukusanyika na kujieleza ni ufunguo muhimu kwa Misri kuelekea katika mpango wake wa kura ya maoni ya katiba itakayofuatiwa na uchaguzi wa wabunge na rais.