Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wataka hatua zichukuliwe haraka baada ya ripoti za mauaji ya watoto Kinshasa :

UM wataka hatua zichukuliwe haraka baada ya ripoti za mauaji ya watoto Kinshasa :

Umoja wa Mataifa leo umetoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuchukua hatua haraka kufuatia ripoti za kusikitisha  za kupotea na kuuawa kwa watoto na vijana yaliyokwenda sanjari na operesheni ya serikali ya kukabiliana na uhalifu mjini Kinshasa.

Kwa mujibu wa ripoti ambazo kwa sasa zinathibitishwa na watu 20 wakiwemo watoto 12 wamearifiwa kuuawa imesema taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na mpango wa Umoja wa mataifa nchini Congo MONUSCO.

Mashirika hayo mawili yamesema taarifa za kusikitisha za kupotea na kuuawa kwa watoto na vijana zinakwenda sambamba na kuanza kwa operesheni Likofi ambayo serikali ya Congo inaiendesha tangu wiki iliyopita kukabiliana na uhalifu unaofanywa na vijana mjini Kinshasa.

UNICEF na MONUSCO wametoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kukomesha vitendo hivyo, na kuhakikisha haki za binadamu zinaheshimiwa kwa mazingira yoyote yale na watoto wanapewa ulinzi maalumu kwa kufuata sheria za Congo na mikataba ya  kimataifa.

Wametaka uchunguzi ufanyike na wahusika kufikishwa kwenye mkono wa sheria.