Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa UM Yemen azuru Sa’ada:

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa UM Yemen azuru Sa’ada:

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed, amezuru mji wa Sa’ada Kaskazini mwa Yemen na kukutana na gava, tume ya rais, tume ya bunge, viongozi wa eneo hilo na  wadau wengine wa misaada ya kibinadamu.

Ziara yake imekuja wakati ambapo machafuko kwaskazini mwaYemenhususan Dammaj na Kitaf yameingia wiki ya sita. Kumekuwa na fursa ndogo saana iliyowezesha kuwahamisha majeruhi 126 walioumia vitani ili waweze kutibiwa, lakini watu wengi zaidi wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.

Bwana Ahmed amesema anasikitika kwamba wafanyakazi wa misaada hawawezi kuwafikia maelfu ya raia katika miji hiyo miwili ambao wanahitaji msaada. Amezitaka pande zote katika mapigano kuruhusu wafanyakazi wa misaada kuwafikia walioathirika , pia amesisitiza pande hizo kuzingatia wajibu wao wa kulinda raia.

Amesema vizuizi vilivyowekwa katika barabara inayoelekea Sa’ada vinazuia mafuta, chakula, madawa na huduma zingine muhimu kuwafikia watu  hususani wakimbizi wa ndani 14,500 walioko katika kambi ya Al Mazrag iliyopo jimbo la Hajjah. Machafuko hayo pia yameathiri watu 29,000 wanaoishi maeneo ya kuzunguka Dammaj na Kitaf.