Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa haraka wahitajika kwa wakulima Ufilipino: FAO

Msaada wa haraka wahitajika kwa wakulima Ufilipino: FAO

Kimbunga Haiyan kimesababisha madhara makubwa nchini Ufilipino lakini madhara hayo yanaweza kuwa maradufu zaidi kwa wakulima iwapo hatua hazitachukuliwa kuwapatia usaidizi wa kuwawezesha kuendelea na kilimo kwa ajili ya kujipatia kipato.

Hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo duniani FAO ambalo linatoa wito kwa mashirika ya utoaji misaada kuchukua hatua za haraka na kuchangisha zaidi ya dola milioni 11 zitakazotelewa kwa watu wanaoishi vijijini kusaidia kuandaa ardhi za kilimo baada ya uharibifu uliosababishwa na kimbunga Haiyan.

Idara ya kilimo nchini Ufilipino imeitaka FAO iongoze shughuli hiyo inayolenga karibu ekari 150,000 na kilomita 80 za mabomba ya unyunyizaji maji mashambani.

Ombi hilo ni kando ya ombi la awali la dola milioni 20 ambalo lilikuwa tayari limetolewa na FAO kuwasaidia wakulima walioathiriwa na kimbunga ili waweze kupanga na kutunza mimeayaona kuhakikisha wamepata mavuno mwakani.

FAO pia imechangisha dola milioni 7  zitakazotumiwa kwa huduma za dharura nchini Ufilipino  ambazo kwa sasa zinagharamiwa na mataifa ya Ubelgiji, Uswisi, uingereza na mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa.