ICC yatengua uamuzi wake kuhusu Kenyatta kufika mahakamani

26 Novemba 2013

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague wanaohusika na kesi dhidi ya Rais waKenya, Uhuru Kenyatta leo wamebadili uamuzi wao ruhusa ya mshtakiwa kutokuwepo mahakamani mfululizo wakati kesi yake inaposikilizwa.

Awali walikuwa wamemruhusu lakini baada ya rufani iliyowasilishwa na kutolewa ufafanuzi wa kisheria, hii leo, Jaji Eboe- Osuji amesema mshtakiwa atapaswa kuwepo mahakamani na kwamba ombi lolote la kusamahewa kuwepo mahakamani litasikilizwa kadri litakavyowasilishwa.

Mahakama imesema kuwa hoja ya rufani iliyowasilishwa tarehe 25 mwezi uliopita kwenye kesi ya Mwendesha mashtaka dhidi ya William Ruto na Joshua Arap Sang imetoa taarifa mpya iliyowezeshwa uamuzi wa awali kutenguliwa.

Ilielezwa kuwa kutokuwepo mahakamani kunaruhusiwa tu katika mazingira ya kipekee na ni lazima ruhusa itolewe pale ambapo ni lazima na si vinginevyo.

Tarehe 18 mwezi Oktoba mahakama ilimpatia ruhusa yenye masharti Kenyatta kutowepo mahakamani mfululizo wakati kesi dhidi ya ikisikilizwa isipokuwa tu wakati wa ufunguzi, utoaji wa ushahidi, siku ya hukumu na siku ambazo mahakama itaagiza awepo.

Kenyatta anashtakiwa kwa makosa matano ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji, ubakaji yanayodaiwa kutendwa wakati wa ghasia zilizoibuka baada ya uchaguzi mkuu waKenyamwaka 2007. kesi yake inaanza kusikilizwa tarehe Tano mwezi Februari mwakani.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter