Kampeni ya chanjo kwa watoto yaanza huko Tacloban: WHO

26 Novemba 2013

Nchini Ufilipino kampeni ya chanjo dhidi ya polio na surua imeanza kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano kwenye mji wa Tacloban ambao ulipigwa zaidi na kimbunga Haiyan . Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kampeni hiyo inalenga kufikia zaidi ya watoto Elfu Thelathini na itahusisha pia utoaji wa matone ya Vitamini A ili kuongeza kinga ya mwili kwa watoto hao dhidi ya magonjwa. Shirika la Afya duniani WHO linasema kazi hiyo inafanyika kwa ushirikiano na serikali ya Ufilipino pamoja na UNICEF na wabia wengine kwenye mji huo ambao madhara ya kimbunga yanatishia afya ya watoto.

Jumanne, watoa chanjo wakiwemo raia wa nchi hiyo na wageni waliweza kutembelea vituo 20 kwenye vituo maalum vilivyowekwa katika makazi ya watu na yale ya muda. Afisa wa UNICEF huko Tacloban Angela Kearney amesema watoto wa eneo hilo wanahitaji kupatiwa kinga zote wanazoweza kupatiwa sasa akisema kuwa watafanya kila wawezalo kufanikisha hilo. Pamoja na chanjo, watoto pia wanachunguzwa utapiamlo.