Sheria mpya ya maandamano Misri inahitaji mabadiliko: UM

26 Novemba 2013

Sheria mpya iliyobuniwa nchini Misri kwa lengo la kudhibiti maanadamno huenda ikawa yenye ukiukaji mkubwa wa haki  ya  kukusanyika kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa. Taaarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Sheria hiyo inazipa idara za usalama  uwezo wa kupiga marufuku mikutano  na kuwazuia waandamanaji  kutoka kwa  tabia ambayo inaweza kutishia usalama au kuvuruga shughuli za raia wengine.

Sheria hiyo inaruhusu matumizi ya vitoa machozi , maji , guruneti za moshi , risasi za mipira na hata risasi halisi katika kuzima maandamano.

Kamishina mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Navi Pillay ameipinga sheria hiyo akisema kuwa inahitaji kufanyiwa marekebisho  kwa kuwa inaweza kutumiwa kwa njia mbaya na idara za usalama na kuruhusu matumizi ya nguzu dhidi ya waandmanaji. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa

 “Mashirika ya umma nchini Misri na watetesi wa haki za binadamu walielezea hisia zao lakini haya yote hayajatiliwa maanani. Linalotia wasi wasi ni vipengee kuhusu matumizi ya nguvu na idara za usalama na vikwazo ikiwemo faini kubwa na hata hukumu za vifo kwa wale ambao watapatikana kukiuka sharia hii. Kumekuwa na visa vya kushangaza kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ambapo utawala umekuwa ukitumia nguvu nyingi dhidi ya waandamanaji hususan visa vilivyotokea tarehe 14 mwezi Agosti eneo la Rabaa al- Adawiya mjini Cairo. Sheria hiyo inastahili kuweka wasi kuwa kulingana na viwango vya kimataifa matumizi ya bunduki yanaweza kufanyika tu wakati inapolazimu ili kulinda maisha.”