Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa 17 vya polio vyabainika Syria:WHO/UNICEF

Visa 17 vya polio vyabainika Syria:WHO/UNICEF

Jumla ya visa 17 vya polio type 1 vimethibitishwa nchini Syria. Visa 15 vimebainika katika jimbo la Deir Al Zour na viwili  kimoja nje ya Damascus na kingine Aleppo, na hivyo kudhihirisha kwamba virusi hivyo vimesambaa.

Hatua za kukabiliana na mlipuko huo katika kanda nzima zinaendelea kuchukuliwa limesema shirika la afya duniani WHO na lile la kuhudumia watoto UNICEF. Nchi saba zinaendesha chanjo ya polio kwa lengo la kuwachanja watoto milioni 22 wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Katika azimio la pamoja nchi zote za Mediteraniani Mashariki zimetangaza kutokomeza polio kama ni hali ya dharura wakitoa wito wa msaada kuhakikisha watoto ambao kwa sasa hawajafikiwa kupata nafasi ya chanjo ya polio.

WHO na UNICEF wanasema wamedhamiria kushirikiana na mashirika yote na kutoa msaada wa kibinadamu unaohitajika kwa Wasyria walioathirika na vita ili kuhakikisha watoto wa Syria wanapata chanjo bila kujali wapi walipo.