Mkutano wa Geneva kuhusu Syria kufanyika Januari: Ban

25 Novemba 2013

Hatimaye tarehe ya mkutano wa pili wa amani kuhusu Syria imewekwa hadhari hii leo mjini New York na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon Ban Ki-Moon akieleza kuwa ni 22 Januari mwakani. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Jumatano ya tarehe 22 Januari 2014 ndio mkutano huo utafanyika mjini Geneva na Ban Ki-moon amewaambia waandishi wa habari kuwa hatimaye kwa mara ya kwanza ujumbe wa serikali  ya Syria na upande wa upinzani watakutana kwenye meza ya mazungumzo na si uwanja wa vita. Ametoa shukrani  kwa waliokesha kutwa kucha kufanikisha mpango huo akisema kuwa njia ya matumaini ambapo pande zote zinakwenda kwenye mazungumzo hayo na uelewa thabiti kuwa mazungumzo ya Geneva ndio njia ya amani ya kuwapatia wasyria matamanioyaoya uhuru, hadhi na usalama wa jamii zote nchini mwao.

Amesema lengo liko dhahiri,

 (Sauti ya Ban)

 “Kutekeleza makubaliano ya Geneva ya mwezi Juni mwaka 2012 ikiwemo kuanzisha kwa maridhiano chombo cha utawala cha mpito chenye mamlaka ya utendaji juu ya jeshi na vyombo vyote vya usalama.”

Amesema mzozo wa Syria bado ni tishio kubwa kwa usalama na amani duniani na kwamba itakuwa ni jambo lisilosameheka iwapo fursa ya sasa haitumiwa ipasavyo kumaliza machungu yanayowapata raia wa Syria ndani na nje ya nchi yao pamoja na uharibifu uliojitokeza.