UNFCCC yazindua ubia mpya na kampuni ya GeSI

22 Novemba 2013

Makubaliano kati ya taasisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa, UNFCC na kampuni ya kimataifa ya suluhu endelevu mtandaoni, GeSi yanalenga kutafuta na kueneza matumizi ya teknolojia zisizo na madhara kwa mazingira. Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya pande mbili hizo ikikariri UNFCCC ikisema kuwa teknolojia ya habari na mawasiliano ina nafasi muhimu katika kupatia suluhu endelevu tatizo la mabadiliko ya tabianchi.

Maafisa waandamizi wa serikali na kampuni binafsi na za umma walioko Warsaw wakizungumza kwenye tukio la utiaji saini makubaliano hayo wamesema ni dhahiri kuwa teknolojia ya mawasiliano inaweza kupunguza matumizi ya nishati, kupunguza gesi chafuzi na hata kujenga uwezo wa kuwa thabiti dhid ya mabadiliko ya tabianchi. Mkutano wa Warsaw kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa unamalizika leo Ijumaa.