Ukatili wa kingono haukubaliki, bila kujali kavalia nini mwanamke: Pillay

22 Novemba 2013

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kaatika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema  kila mmoja anatakiwa kutimiza jukumu lake la kukomesha imani zinazosaidia kuendeleza mazingira ambayo yanafanya ukatili dhidi ya wanawake kuonekana kama jambo la kukubalika, au kwamba wanawake hao wanastahili kufanyiwa ukatili. Amesema ukatili wa kingono hauwezi kukubalika kamwe, bila kujali mwanamke kavalia nini.

Bi Pillay amesema hayo katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake, ambayo ni Jumatatu Novemba 25. Amesema kuwa ukatili dhidi ya wanawake umeendelea kuwa mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya nyakati za sasa, akisema ni jambo la aibu kuwa hata wakati huu, kwa wanawake na watoto wengi wa kike, ukatili dhidi yao umewazingira pembezoni mitaani, maeneo ya ajira, na hata nyumbani kwao kwenyewe, akiongeza kuwa aghalabu hawapati haki.

Bi Pillay ametaja mifano ya ubakaji wa mtoto wa miaka 16 kwenye mji wa Busia nchini Kenya, ambaye baada ya kubakwa mnamo mwezi Juni, polisi waliwaamuru wabakaji kukata nyasi kama adhabu, na ule wa New Zealand, ambako msichana wa miaka 13 alipokwenda kuripoti kisa cha kubakwa na wavulana watatu, moja ya maswali aloulizwa kwanza lilikuwa: “ulikuwa umevalia nini?”

Bi Pillay amesema uhalifu kama huo hutendeka kila siku katika nchi nyingi kote duniani, ingawa hauripotiwi, kwani wanawake katika jamii nyingi wanaona aibu kuripoti visa vya ukatili wa kingono kwa polisi