Wakimbizi wa DRC waanza kurejea nyumbani kutoka Uganda

22 Novemba 2013

Takriban wakimbizi elfu saba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliotorokea nchi jirani ya Uganda kufuatia makabiliano kati ya jeshi la serikali ya DRC na waasi wa M23, wamerejea makwao baada ya utulivu kurejea.

John Kibego wa redio washirika ya Spice FM, ana ripoti kamili kutoka Uganda.

(Tarifa ya John Kibego)

Wakimbizi 3,275 pekee ndio wamesalia kati ya wakimbizi 10,500 waliopokewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) katika wilaya ya Kisoro, kulingana na hesabu ya tarehe 28 mwezi Oktoba.

Walikimbia mapambano makali yaliyoshuhudiwa kwenye miji ya Rutshuru, Kiwanja, na Bunagana kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali ya Kinsasha likisaidiwa na jeshi la kujibu mashambulio la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita.

Lucy Beck, msemaji wa UNHCR wa eneo la Kusini Magharibi mwa Uganda amesema, watu 1,283 wa waliogopa kurejea nyumbani tayari wamesafirishwa hadi kwenye kambi ya wakimbizi ya Rwamwanje.

(Sauti ya Lucy Beck)

Amesema wanapanga msafara mwingine kutoka kambi ya muda ya Nyakabambe hadi Rwamwanje wa wakimbizi 1992 ambao wamekuwa wakiangaliliwa hapo.

(Sauti ya Lucy Beck)`

Kwanzia mwezi April mwaka jana, kambi ya Rwamwanje imepokea wakimbizi 6,151 wakitoroka fujo katika jimbo la Kivu ya Kaskazini Mashariki mwa DRC.

Mipango ya mazungumzo ya amani kati ya M23 na DRC mjini Kampala haijatoa matumaini kwa sababu serikali ya Kinsasha inasema haina muda wa kuzungumza na waasi waliozidiwa nguvu.