UNHCR yaharakisha misaada kwa waathirika wa kimbunga

20 Novemba 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wakimbizi UNHCR limeanza kusambaza misaada ya dharura kwa waathirika kwa kimbunga Haiyan baada ya ndege yake ya mizigo kuwasili katika uwanja wa Tacloban .

Misaada hiyo imepekekwa katika eneo la San Jose eneo ambalo limeaathiriwa vibaya na kimbunga hicho.

Kumekuwa na uharibifu mkubwa katika eneo ka San Jose huku baadhi ya nyumba zikiwa katika hali mbaya na nyingine kusombwa kabisa na kimbunga hichi kilichotokea Novemba 8. Juhudi zinazofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kiraia zimesaidia kuleta matumani kwa familia nyingi ambazo baadhi yao bado ziko katika hali mbaya.

Ili kurahisisha shughuli za utoaji misaada UNHCR imeandaa utaratibu unaowataka waathirika kusimama katika mistari maalumu na baadaye hupatiwa mahutaji wanayostahili. Lakini watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo wanawake na wale wanaotunza familia kubwa wameandaliwa utaratibu wa kipekee ambao hurasisha utoaji huduma.