Baraza la Usalama lamulika hali CAR na waasi wa LRA

20 Novemba 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana leo kujadili hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku masuala ya usalama na uhalifu unaovuka mipaka yakimulikwa, vikiwemo vitendo vya waasi wa LRA. Joshua Mmali na taarifa kamili:

(TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

Wakati wa Mkutano wake hii leo, Baraza la Usalama limesikiliza ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu shughuli za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, UNOCA, na kuhusu maeneo yaloathiriwa na kundi la waasi la LRA. Akiiwasilisha ripoti hiyo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa UNOCA, Abou Moussa, amesema kuwa hali mbovu ya usalama Jamhuri ya Kati inatishia usalama wa ukanda mzima

ABOU MOUSSA

“Ukosefu wa usalama na utulivu katika Jamhuri ya Kati bado inatishia uslama na hali ya kibinadamu kwa nchi jirani zake. Uwezekano wa mgogoro nchini humo kuvuka mipaka na kuingia ukanda mzima bado ni dhahiri. Pili, uhalifu wa kuvuka mipaka bado ni changamoto kubwa kwa usalama wa Afrika ya Kati.”

Kuhusu waasi wa LRA, amesema kuwa ingawa nguvu za kundi hilo la LRA zimepungua, bado linatoa tishio kwa usalama

“Hatua za kijeshi zimeidhoofisha LRA na kuilazimu kuandama tu mbinu za kujinusuru. Hata hivyo, mashambulio ya hivi karibuni Sudan Kusini ni ukumbusho kuwa kundi hilo bado ni tishio kubwa na lisilotabirika kwa jamii zote za ukanda huo.”