Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya watoto duniani yaadhimishwa leo wakati suala la kiweka wazi dhuluma dhidi ya watoto likipewa kipaumbele

Siku ya watoto duniani yaadhimishwa leo wakati suala la kiweka wazi dhuluma dhidi ya watoto likipewa kipaumbele

Wakati siku ya watoto inapoadhimishwa ambapo haki za watoto zinakumbukwa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF linataka maslahi ya watoto kuangaziwa zaidi na kila nchi hasa wale wanaokumbwa na dhuluma na mateso yasiyotambuliwa . Taarifa ya Flora Nducha inafafanua zaidi.

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF Antony Lake amesema kuwa mara nyingi watoto hudhulumiwa kwenye visa ambavyo havitambuliwa na vibaya zaidi akiongeza kuwa ni wajibu wao kuhakikisha kuwa yote haya yamewekwa wazi.

Amesema serikali zinahitaji kubuni sheria za kuzuia dhuluma dhidi ya watoto ambazo ni za aina nyingi zikiwemo za nyumbani, za kimapenzi na adhabu kali wanazopitia watoto na zinazofanyika wakati wa mizozo na vita.

Kati ya hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuzuia dhuluma hizo ni pamoja na kuwasaidia wazazi, na wale wanaowatunza watoto, kuwapa watoto uwezo wa kujitetea na kubadili mienendo na tabia zinazoruhusu watoto kudhulumiwa pamoja na kubuni na kutekelezwa kwa sheria zinazowalinda watoto.