Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa COP19 wafunguliwa, viongozi watakiwa kufikiria kwa mapana zaidi

Mkutano wa COP19 wafunguliwa, viongozi watakiwa kufikiria kwa mapana zaidi

Mkutano wa ngazi ya juu wa mabadiliko ya tabia nchi, umefunguliwa rasmi huko Poland ambapo Umoja wa Mataifa umetaka viongozi kutokuwa wabinafsi katika fikra za mabadiliko ya tabianchi, huku shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa likitoa ripoti inayosema kuwa gharama za kukabili mabadiliko ya tabianchi Afrika itaongezeka iwapo hatua hazitachukuliwa. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

 (Ripoti ya Assumpta)

Mjini Warsaw,Poland katika ufunguzi wa mkutano huo,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametumia hotuba yake kueleza kuwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri shahiri, iwe kwenye nchi tajiri na nchi maskini. Ametolea mfano ukame wa kupindukia ukanda wa Sahel unaokwamisha jitihada za maendeleo na kuyeyuka kwa barafu hukoIceland kunakotishia kuzama kwa kisiwa hicho. Mifano ni mingi lakini akatoa wito wa umoja kwenye makubaliano mapya kuhusu mabadiliko ya tabianchi ya mwaka 2015 hukoParis. Hivyo akawaeleza maraisi na viongozi wengine wanaoshiriki mkutano huo..

“Nawaomba nyote mliokuja kuchukua hatua na vitendo vya kijasiri. Tunahitaji uongozi wenu wa kisiasa wakati huu muhimu. Naomba mfikirie kile mnachotaka kukumbukwa nacho. Msipange kwa ajili ya nchi yetu, bali pia mfikirie jirani yako na jirani ya jirani yako. Usijenge kwa ajili ya leo tu, bali kwa ajili ya watoto wako na watoto wao.”

Mapema UNEP imezindua ripoti inayokadiria kuwa Afrika inaweza ikaingia gharama ya dola Bilioni 350 kila mwaka ifikapo mwaka 2070 iwapo wakati huu itashindwa kutekeleza mipango ya kupunguza athari za uharibifu wa mazingira ikiwemo kuhakikisha kiwango cha nyuzi joto mbili kilichozidi, hakitaongezeka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo mjiniWarsaw, Waziri wa Tanzania anayehusika na Mazingira Dr.Terezya Huviza amesema Afrika haiwezi kucheza mchezo hatari wa kupuuzia kutekeleza majukumu yake hasa wakati huu ambapo idadi ya watu inaendelea kuongezeka na kufikia bilioni 2 mwaka 2050.