Licha ya matumaini ya maendeleo, kuna walakin Sudan Kusini: UM

18 Novemba 2013

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS, Hilde Johnson, ameliambia Baraza la La Usalama kuwa licha ya dalili za matumaini ya kujikwamua na kujiimarisha, taifa la Sudan Kusini bado lipo kwenye barabara ya misukosuko.

Bi Johnson amesema taifa hilo limekabiliwa na changamoto kubwa tangu lijipatie uhuru, ingawa kuna fursa mpya za kulijenga taifa na kuimarisha uwajibikaji.

Amesema serikali imepata ugumu kuimarisha mamlaka yake kote nchini, akitaja jimbo la Jonglei kama mfano wa hali inayoendelea kutia waisiwasi, licha ya utulivu kidogo wakati wa msimu wa mvua.

Bi Johnson pia amekitosa kidole cha lawama vikosi vya usalama nchini humo

Tabia za vikosi vya usalama inaendelea jambo la kutia hofu, iwe kuhusiana na haki za binadamu au visa vya ghasia na kuwatelekeza wahudumu wa Umoja wa Mataifa, wanadiplomasia na wananchi wa kawaida. Sudan Kusini inaendelea kukumbana na changamoto kubwa sana katika kulinda na kuendeleza haki za binadamu. Baadhi ya vitendo vinavyotekelezwa ni kuwakamata na kuwazuilia watu ovyo, matumizi ya nguvu kupindukia na mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na vikosi vya usalama.”

Amesema pia kuna visa vya ukandamizaji wa haki za kujieleza na kujumuika, huku akiahidi kuwa UNMISS inaendelea kuchunguza ripoti za madai ya ukiukwaji huu wa haki, na itaongeza utoaji wa ripoti kama hizo.

Akizungumza baada ya Bi Johnson, Mwakilishi wa Kudumu wa Sudan Kusini kwa Umoja wa Mataifa, amelishukuru Baraza hilo na Umoja wa Mataifa kwa mchango wake kwa taifa lake, na kukiri kuwa bado wana kazi nyingi ya kufanya.

Jamhuri ya Sudan Kusini inatambua kuwa inakabiliwa na changamoto kubwa katika kujenga taasisi zake, kulinda hatua zilizopigwa katika kutafuta demokrasia na kuwalinda raia, miongoni mwa mambo mengine. Hata hivyo, ndoto yetu ni dhahiri: Sudan Kusini imara, yenye amani, maendeleo ya kiuchumi, na inayozingatia kuendeleza haki za binadamu na misingi ya kibinadamu, ingawa tunakubali kikamilifu kuwa hatuna uwezo wa tunahitaji kuwa nao, ili kufikia ndoto hii haraka tunavyotaka.”