Moshi wa chuki dhidi ya binadamu bado unafuka, tusikubali: Ban

18 Novemba 2013

Auschwitz-Birkenau siyo tu eneo lenye orodha ya waliokumbwa na mauaji ya kimbari dhidi ya wayahudi, bali pia ni eneo ambapo wahanga walihifadhi ujasiri wao na matumaini. Ni kauli ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliyotoa Jumatatu baada ya kutembelea kambi hiyo iliyokoPoland ambayo ilitumika kwa mauji ya halaiki.

Bwana Ban ametumia fursa ya ziara hiyo na kusema kamwe tukio la aina hiyo lisirudie tena. Amesema kwa wahanga anatoa hakikisho kuwa kamwe tukio hilo halitasahaulika na kwa mustakhbali wa dunia amesema ni jukumu la kila mmoja kujenga dunia ya amani, yenye usawa na utu kwa kila mtu. Hata hivyo akatoa angalizo.

 (Sauti ya Ban)

 "Hata hii leo twaona moshi ukifuka! Misingi ya chuki dhidi ya wayahudi inaendelea kuthibitika maeneo mbali mbali duniani. Barani Ulaya na kwingineko, wahamiaji, waislamu, waroma na makundi mengine madogo yanakumbwa na ubaguzi unaozidi kuchipukia na mara chache kupata watetezi. Ulimwengu usisahau au kukana au hata kupuuza mauaji ya kimbari dhidi ya wayahudi. Tunapaswa kuendelea kuwa macho. Na tunapaswa kuongeza jitihada zaidi na zaidi kuendeleza usawa na aina zote za uhuru.”

Miongoni mwa wageni katika ziara kwenye kambi hiyo alikuwa Marion Turski, mmoja wa wahanga wa mauaji ya kimbari ambaye pia ni Makamu Rais wa kamati ya kimataifa ya Auschwitz.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter