Siku ya viwanda barani Afrika kuadhimishwa tarehe 22 mwezi huu

18 Novemba 2013

Siku ya viwanda barani Afrika yenye kauli mbiu ubunifu wa ajira na maendeleo ya kibiashara ikiwa ni njia ya kuchochea maendeleo barani Afrika itaadhimishwa mjini New York tarehe 22 mwezi huu.

Siku hii iliyobuniwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1989 inatoa hamasisho kuhusu wajibu wa viwanda kwenye maendeleo ya bara la Afrika na pia inavutia uwekezaji wa kimataifa kutoka kwa washikadau tofauti zikiwemo serikali, sekta za kibinafsi na mashirika ya umma.

Shirika la maendeleo ya kiviwanda la Umoja wa Mataifa UNIDO litaandaa sherehe hiyo kwa ushirikiano na mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika na mwangalizi wa Muungano wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa.

Maadhimisho ya mwaka huu yatahusisha vikao vya mashauriano vya wataalamu kutoka kwa sekta za kibinafsi na umma ambapo watabadilishana mawazo kuhusu biashara na ajira.