Nchi wanachama watakiwa kushirikiana na Somalia kupambana na uharamia:

18 Novemba 2013

Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamechagizwa kuendelea kushirikiana na serikali ya Somalia kuhakikisha wanatokomeza tatizo la uharamia. Joshua Mmali na taarifa kamili:

(TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

Ni rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Novemba, Balozi Liu Jieyi wa Uchina, akitangaza matokeo ya kura kuhusu kupambana na uharamia kwenye pwani ya Somalia.

 

Kwa azimio hilo 2125, (2013), nchi zote wanachama zimeombwa kushirikiana na mamlaka za Somalia katika vita dhidi ya uharamia na wizi wa kutumia silaha baharini, kwenye pwani ya nchi hiyo.

Baraza hilo la Usalama pia limeongeza muda wa idhini zilizotolewa katika maazimio ya awali kwa nchi na mashirika ya kikanda yanayoshirikiana na Somalia kupambana na uharamia kufanya hivyo.

Kwa azimio hilo pia, Baraza la Usalama limeamua kuwa vikwazo vya silaha vilivyowekwa zamani dhidi ya Somalia katika azimio 733 la mwaka 1992 na kufanyiwa marekebisho hadi mwaka 2002, halihusiki na usafirishaji wa silaha na vifaa vya kijeshi vinavyolenga kutumiwa na nchi wanachama kwa jukumu la kupambana na uharamia na wizi wa baharini.