Kimbunga Haiyan ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi:Ban

Kimbunga Haiyan ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiwa ziarani nchini Lithuania amekutana na kuzungumza na wasomi na viongozi wa kijamii katika chuo kikuu La Vytutas Magnus nchini humo ambapo amesema changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni tishio kubwa la mustakabali wa dunia.

Akitolea mfano wa kimbunga  Haiyan kilichoikumba Ufilipino hivi karibuni na kusababisha upotevu wa maisha na uharibifu mkubwa Katibu Mkuu Ban amesema hali ya hewa sio jambo lenye madhara kesho bali ni leo na kwamba kimbunga hicho ni tahadhari ya madhara yanayoweza kujitokeza ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa.

Bwana Ban pia amezungumzia ukosefu wa amani duniani akiangazia mgogoro wa Syria ambao amesema ni changamoto kubwa ya amani na usalama duniani kwa sasa.

Katika mkutano huo Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alitunukiwa shahada ya heshima ambapo amesema hiyo ni ishara kuwa chuo kikuu hicho kimetambua kazi inayofanywa na Umoa huo kupitia wafanyakazi wake duniani wanojituma katika kukuza amani na ustawi wa binadamu.