Tutumie hatua rahisi kuepusha vifo vya watoto njiti: Balozi Kasese-Bota

17 Novemba 2013

Mtoto mmoja kati ya watoto Kumi huzaliwa kabla ya muda yaani njiti na katika matukio mengi hufariki dunia. Ni takwimu zilizotolewa wakati wa kongamano tangulizi kuhusu siku ya kimataifa ya kimataifa ya kuhamasisha umma kuhusu watoto njiti na hatua za kuchukua kuboresha afya zao ili waepuke magonjwa nyemelezi kama vile numonia na kuhara. Siku hiyo ni leo tarehe 17 Novemba na ujumbe ni  Kinga na malezi kwa watoto njiti na mkakati mpya kwa watoto wachanga. Miongoni mwa wazungumza wakati wa kongamanohilolililofanyika kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa kudumu waZambiakwenye Umoja huo Dokta Mwamba Kasese-Bota ambaye pamoja na kusema kuwa suala la watoto njiti ni kubwa lakini bado halitiliwi maanani, alitoa ushuhuda.

(Sauti Dokta Kasese-Bota)

“Nina binti wa miaka saba ambaye alizaliwa njiti wakati ujauzito  una wiki 23. Alikuwa ni pacha wa pili. Pacha wa kwanza alifariki dunia akiwa na siku nne baada ya kuzaliwa.”

Balozi Kasese-Bota akasema kuwa suala la watoto njiti na changamoto wanazokabiliana nazo wao pamoja na mama zao ni tatizo bado nchiniZambiana nchi nyingine zinazoendelea ilhali kuna njia rahisi za kupatia suluhu changamoto hizo na kuboresha afya za watoto hao.

(Sauti ya Dokta Kasese-Bota)

Njia hizo ni pamoja na ile iitwayo Kangaroo ya kumpatia joto mtoto, na sindano maalum anayochomwa mama anayepata uchungu mapema, kuzuia uambukizi pamoja na dawa kuzuia na kukabiliana na maambukizi. Nchini Zambia suala la watoto njiti bado ni tatizo na takwimu za vifo kwa watoto njiti ni za juu. Lakini serikali imechukua hatua kwa kuandaa mfumo wa kushughulikia masuala ya watoto wachanga ikiwemo hilo la njiti.”

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la Afya, WHO na lile la watoto UNICEF yanaongoza kampeni ya kimataifa ya mkakati wa afya kuhusu Mtoto mchanga utakaozinduliwa  mwezi Mei mwakani, Mkakati huo utawezesha watunga sera na wadau wengine kuchukua hatua kuharakisha mipango ya kuboresha afya ya mama na mtoto ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ya makundi hayo.