Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa mafuta waathiri jitihada za utoaji misaada Ufilipino:UM

Uhaba wa mafuta waathiri jitihada za utoaji misaada Ufilipino:UM

Nchini Ufilipino ambako wakati mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiendelea na jitihada za kutoa misaada kwenye maeneo yaliyokumbwa na kimbunga Haiyan nchini Ufilipino uhaba mkubwa wa mafuta umekwamisha jitihada za kuwafikia mamilioni ya watu walioathiriwa na kimbunga hicho. Jason Nyakundi na taarifa kamili.

(TAARIFA YA JASON NYAKUNDI)

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema kuwa hata kama misaada inaendelea kuwasili nchini Ufilipino, kuisafirisha kwa wale wanaoihitaji inachukua muda mrefu kutokana na kuwepo uhaba wa mafuta. Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF linasema kuwa mafuta linayo yataliwezesha tu kutoa huduma kwa muda wa siku mbili huku shirika la mpango wa chakula duniani WFP nalo likisema kuwa malori yaliyo na misaada yamekwama kwenye uwanja wa ndege wa Tacloban kutokana na uhaba wa mafuta. Elisabeth Byrs ni msemaji wa WFP mjini Geneva.

“Mafuta yataisha siku chache zijazo. Lakini vile WFP imekodisha malori kadha, WFP inatafuta mbinu za kupata mafuta. Tunahitaji hifadhi ya mafuta na tutafanya hivyo wakati wasimamizi wa masuala ya usafiri watafanya mashauriano na utawala wa Ufilipino. Siku ya Alhamisi tutasambaza biskuti kwa watu 5000 kwenye uwanja wa ndege wa Tacloban. Usafirihaji wa biskuti kwa wale walioathirika utaanza leo. Ifikapo mwishoni mwa Alhamisi migao 34,000 ya chakla itakuwa imesambazwa kwenye mkoa wa Laite. Migao hiyo ya WFP inajumuisha kilo tatu za mchele na imewafikia watu 170,000”

Idadi ya watu walioathiriwa na kimbunga Haiyan imeongezeka hadi watu milioni 11.8 huku watu 920, 000 wakiwa wamehama makwao na sehemu nyingi zikiwa hazifikiki