Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asifu hatua za maendeleo Latvia

Ban asifu hatua za maendeleo Latvia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amelipongeza taifa la Latvia kwa kuendeleza haki za binadamu, kuwapa wanawake nguvu na kuendeleza usawa wa jinsia. Bwana Ban amesema hayo katika mkutano na waandishi habari wakati wa ziara yake nchini humo, akiongeza kuwa taifa hilo huchangia mara kwa mara kwa ajenda ya kimataifa ya amani, maendeleo na haki za binadamu.

“Nafurahia mchango wa Latvia katika kutusaidia kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ifikapo mwaka 2015, na kwa kuweka mpango wa maendeleo baada ya hapo. Nimemwomba rais kuendeleza hata zaidi ushirikiano wa Latvia na Umoja wa Mataifa.”

Katibu Mkuu amesema yeye na Rais Andris Bērziņš  wa Latvia wamejadili pia masuala mengine, yakiwemo mzozo unaoendelea nchini Syria, na juhudi za kupata suluhu la kisiasa, pamoja na mustakhbali wa Afghanistan na mdororo wa kiuchumi wa kimataifa.

 “Latvia imeonyesha ukuaji imara wa uchumi, licha ya mdororo wa kiuchumi. Nimempa heko rais kuhusu mchango wa Latvia kama mfano wa kuigwa, kwa kubadilika na kuwa jamii iliyoendelea nay a kidemokrasia katika miongo michache.”