Plumbly azuru wakimbizi wa Syria Bekaa Lebanon:

13 Novemba 2013

Mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Lebanon Derek Plumbly, leo amezuru maeneo ya Zahleh na Joub Jennin Magharibi mwa bonde la Bekaa nchini Lebanon ili kuangalia hali ya wakimbizi wa Syria na jamii inayowahifadhi.

Mratibu huyo pia amekwenda kufuatilia juhudi za shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa mataifa UNHCR na serikali ya Lebanon na wadau wengine katika kukidhi mahitaji ya wakimbizi hao. Akiwa nchini humo bwana Plumby amekutana na wawakilishi wa UNHCR na mashirika mengine ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu mjini Zahleh ambao wamempa taarifa juhudi zao zilizoanza mwanzoni mwa mwezi Novemba za kuhakikisha msaada wa lazima unapatikana katika msimu wa majira ya baridi unaokuja .

Ametembelea miradi miwili huko Joub Jennin, inayotekelezwa kwa pamoja na UNDP, UNHCR na manispaa ya mji huo ukiwemo wa ujenzi wa mtambo wa maji, ambao utasaidia sana mahitaji ya wakimbizi hao kwa muda mrefu. Bwana Plumby amekutana pia na wakimbizi wa Syria kwenye makazi ya Kob Elias na kusikiliza hadithi za machungu ya kutawanywa kwao na machafuko yanayoendelea Syria. Amessisitiza kuwa Lebanon na jumuiya ya kimataifa wataendelea kuwasaidia wakimbizi hao.