Mpango mpya kuboresha huduma za uzazi wa kupanga baada ya kujifungua mimba: WHO

13 Novemba 2013

Shirika la Afya Duniani, WHO, limezindua mpango mpya wa kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi wa kupanga kwa akina mama katika miezi 12 ya kwanza baada ya kujifungua, ambao unawalenga wahudumu wa afya na watunga sera. Kwa mujibu wa WHO, mimba zinazokaribiana sana au zisizotarajiwa ni tishio la kiafya kwa mama na mtoto, na kwamba kuweka pengo la angaa miaka miwili kabla ya mimba nyingine kunaweza kuepusha asilimia 10 ya vifo vya utotoni na takriban kuepusha kifo kimoja kati ya vitano miongoni mwa watoto wenye umri kati ya mwaka mmoja hadi minne. Mpango huo ambao umezinduliwa katika kongamano la kimataifa kuhusu uzazi wa kupanga mjini Addis Ababa, Ethiopia, unanuia kuitikia mahitaji kwa ngazi zote za huduma za afya, ili kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa akina mama mara tu baada ya kujifungua. Takwimu kutoka nchi 27 zinazoendelea zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya wanawake wanataka kujiepusha na mimba kwa angaa miaka miwili baada ya kujifungua, lakini asilimia 65 kati yao hawatumii mbinu za kuzuia mimba.