Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa wa Pneumonia wangoza kwa vifo miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano duniani

Ugonjwa wa Pneumonia wangoza kwa vifo miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano duniani

Ugonjwa wa Pneumonia unaongoza kwa kusababisha vifo vingi zaidi miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano duniani ambapo husababisha zaidi ya vifo milioni moja kila mwaka. Lakini hata hivyo vifo hivyo vinaweza kuzuiwa. Taarifa kamili na Flora Nducha

(Taarifa ya Flora Nducha) 

Huku nchi zikiadhimisha siku ya ugonjwa wa Pneumonia duniani hii leo muungano wa GAVI, shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF pamoja na shirika la afya duniani WHO yanashughulikia hatua muhimu ambazo zinaweza kuzuia vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa Pneumonia miongoni mwa watoto. Mkuu wa idara na afya kwenye shirika la UNICEF Dr Mickey Chopra anasema kuwa kwa kila sekunde 30 mtoto aliye chini ya miaka mitano huaga dunia kutokana na ugonjwa wa Pneumonia.

Masuala mengi huchangia ugonjwa wa Pneumonia na hakuna njia moja ambayo inaweza kuuzuia ugonjwa huo . Kati ya hatua ambazo ikiwa zitafuatilia zinaweza kuuzuia ugonjwa huo ni pamoja na Kumnyonyesha mtoto kwa kipindi cha miezi sita mfululizo na kuendela kumyonyesha huku akipewa chakula kingine hadi atimie miaka miwili. Chanjo dhidi ya magonjwa yakiwemo ugonjwa wa Surua, kuwepo kwa maji safi ya kunywa, usafi na kunawa mikono.