Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani wajawazito 200,000 wahitaji msaada Ufilipino baada ya kimbunga Haiyan: UNFPA

Takribani wajawazito 200,000 wahitaji msaada Ufilipino baada ya kimbunga Haiyan: UNFPA

Madhara ya kimbunga Haiyan nchini Ufilipino yanazidi kuwa dhahiri shairi kila uchao ambapo Shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA limemulika afya ya uzazi ikisema wajawazito Laki mbili wanahitaji msaada wa haraka baada ya kuathirika na kimbunga hicho. Taarifa ya shirika hilo limetolea mfano mjamzito mmoja huko Tacloban City ambaye alilazimika kujifungulia eneo moja la Uwanja wa Ndege baada ya kushindwa kupata hospitali. Madaktari waliomsaidia mama huyo Emily Sagalis wamesema licha ya kwamba alijifungua salama lakini yeye na mwanae wako hatarini kupata maambukizo kutokana na kushindwa kupata dawa muhimu kama zile za kuzuia maambukizi. UNFPA imesema mtandao wa huduma za afya umesambaratishwa na kimbunga hicho na halikadhalika wahudumu wa afya. Hivi sasa shirika hilo linahamasisha misaada pamoja na watoa huduma ili waweze kuchukua hatua za haraka kupatia jawabu hali hiyo na hatimaye kuokoa maisha ya wanawake na watoto wao.