Wajumbe wa UM wasikitikia mkwamo wa mazungumzo ya Kampala

11 Novemba 2013

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu nchi za Maziwa Makuu, Mary Robinson, Mwakilishi wa Marekani kwenye nchi hizo na DRC, Russ Feingold, Mwakilishi wa Umoja wa Afrika, AU, Boubacar Diarra na Mwakilishi wa Muungano wa Ulaya, EU Koen Vervaeke, pamoja na Mwakilishi wa Katibu Mkuu katika DRC, Martin Kobler, wametoa taarifa ya kuelezea masikitiko yao kuhusu mkwamo wa mazungumzo ya amani ya Kampala leo, ingawa pande husika hazijataja kutofautiana kuhusu vipengee muhimu vya mswada wa makubaliano.

Hata hivyo, makubaliano kuhusu utaratibu hayajafanyika. Wajumbe hao wamesema, licha ya kuwepo mabadiliko katika shughuli za kijeshi, ni muhimu kuwa mazungumzo ya kisiasa yahitimishwe, na hivyo kutoa wito kwa pande husika ziafikiane kuhusu tofauti zilizopo kuhusu jinsi mswada wa makubaliano ulivyoandikwa, na kuendeleza kutafuta suluhu la amani kwa mzozo wa DRC.

Wajumbe hao pia wamesisitiza kuwa suluhu lolote lile ni lazima litoe nafasi ya kuhakikisha uwajibikaji kwa wale ambao wametenda uhalifu wa kivita, uhalifu wa kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukiwemo ukatili wa kingono, usajili wa watoto katika vita, na ukiukwaji mwingine mbaya zaidi wa haki za binadamu.