Mahakama ya ICJ yaikabidhi Cambodia hekalu la Preah Vihear

11 Novemba 2013

Mahakama ya dunia, ICJ, ambayo ndicho kiungo cha sheria cha Umoja wa Mataifa, imetoa uamuzi wake kuhusu kesi iloamuliwa mnamo Juni 15 mwaka1962 kati ya Cambodia na Thailand kuhusu hekalu la Preah Vihear.

Ingawa iliamuliwa mnamo mwaka 1962 kuwa hekalu hilo lilikuwa kwenye ardhi ya Cambodia, bado kulikuwa na hali ya kukanganisha kuhusu vipengee fulani vya maamuzi hayo. Katika hali hiyo, Cambodia ilitoa ombi kwa mahakama ya dunia iufanyie ufafanuzi uamuzi huo.

Katika uamuzi kwa kauli moja basi, mahakama hiyo imesema eneo zima la hekalu la Preah Vihear lipo kwenye ardhi na ndani ya mipaka ya Cambodia, na hivyo basi, Thailand inatakiwa kuondoa vikosi vyake vya kijeshi na polisi, au walinzi na watunzaji wake wengine walioko hapo. Hekalu hilo linapatikana karibu na mpaka kati ya nchi hizo mbili, Cambodia ikiwa kusini, na Thailand kaskazini.