Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gesi chafu na majanga vyamulikwa kwenye mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Gesi chafu na majanga vyamulikwa kwenye mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Kikao cha kumi na tisa cha mkutano wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi umeanza leo mjini Warsaw, Poland, ambako viwango vya gesi ya kaboni angani na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi vimemulikwa. Joshua Mmali na taarifa kamili

TAARIFA YA JOSHUA

Akiufungua mkutano huo, Katibu Msimamizi wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC, Christiana Figueres amesema kikao hicho kinaanza wakati hewa wanayopunga wanadamu sasa ina vipimo vya juu vya kaboni, huku janga la kimbunga Haiyan likikumbusha kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi.

Bi Figueres amesema mabadiliko ya tabianchi yameweka uwanja usio sawa kwa vizazi vijavyo. Amesema hali hii inaweza kubadilishwa, kwani sasa juhudi zaidi zinafanywa, na kuna sababu nyingi za kutakiwa kuchukua hatua, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi zinafahamika, siyo tu dhidi ya mazingira, bali pia kwa usalama, nishati, kiusalama na kwa uongozi. Amesema kuna utashi wa kisiasa na uungwaji mkono wa umma, na hivyo vinatoa nafasi ya kuchukua hatua sasa.

Amesema mkataba mpya wa kimataifa kuhusu tabianchi unakaribia, na hivyo basi nchi wanachama zinatakiwa kuongeza kasi ya kufanya mabadiliko na kushirikiana ili kupata ufanisi ifikapo mwaka 2015, na kuongeza kuwa mkutano huo wa Warsaw unatoa fursa nzuri.