Baraza la Usalama lalaani shambulio la kigaidi Somalia

10 Novemba 2013

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulio la bomu lililofanyika Ijumaa kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, shambulio ambalo kundi la kigaidia la Al-Shabaab limedai kuhusika nalo na limesababisha vifo vya watu kadhaa na majeruhi. Taarifa ya baraza hilo imekariri wajumbe wakituma salamu za rambirambi kwa familia na wananchi pamoja na serikali ya Somalia huku wakisema wanaunga mkono kwa dhati mchakato wa amani na maridhiano nchini Somalia. Wajumbe wamesema wameazimia kuunga mkono jitihada za kimataifa za kuondoa kitisho cha Al Shabaab nchini Somalia na kwenye eneo lote. halikadhalika wamerejelea kauli yao kwamba ugaidi ni kitisho kikubwa kwa amani na usalama duniani na kwamba kitendo chochote cha aina hiyo hakiwezi kuhalalishwa kwa misingi yoyote ile na popote pale kinapofanyika na wameazimia kuutokomeza kwa mujibu wa majukumu ya baraza hilo yalivyoainishwa kwenye mkataba ulioanzisha Umoja wa Mataifa. Taarifa hiyo pia imekariri wajumbe wakisema kuwa shambulio la kigaidia nchini Somalia halitapunguza kasi ya baraza ya kusaidia mchakato wa amani, utulivu na maridhiano nchini humo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter