Botswana na Rwanda zatoa msukumo wa kufanyia marekebisho Baraza la Usalama

8 Novemba 2013

Mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Baraza la Usalama umeingia siku yake ya pili, hukuRwanda na Botswana zikiongeza sauti zao kwa wito wa kutaka Baraza la Usalama lifanyiwe marekebisho.

Akiongea wakati wa mjadala huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Botswanakwenye Umoja wa Mataifa, Charles Thembani Ntwaagae amesema ujumbe waBotswanaunaazizia mno suala la kulifanyia marekebisho Baraza la Usalama, hususan kwenye suala la usawa katika uwakilishi.

Amesema, huku Baraza hilo la Usalama likiwa ndilo kiungo muhimu zaidi cha Umoja wa Mataifa, chenye wajibu wa kuendeleza amani na usalama kimataifa, inasikitisha kuwa tangu liundwe mnamo mwaka 1945, bado halina uwakilishi wa kijografia na kidemokrasia wa wanachama wa Umoja wa Mataifa.

“Ni jambo lisiloeleweka kuwa Afrika inabaki ndio pekee isiyo na uwakilishi katika  taasisi kama hiyo, ambayo uhalali na nguvu zake ni lazima zitokane na wanachama wake wote. Huku maeneo mengine ya ulimwengu yakiwa yana uwakilishi na nafasi katika Baraza hilo, Afrika bado imetengwa na kuchukuwa kiti cha nyuma, bila sauti, bila nguvu na bila uwepo wa ushawishi katika maamuzi muhimu yanayofanywa na taasisi hii yenye nguvu”

Naye Mwakilishi wa Kudumu waRwandakwenye Umoja wa Mataifa, Eugene-Richard Gasana, amesema kuanza harakati za kufanyia Baraza la Usalama marekebisho kunalenga kuonyesha hali halisi ya nyakati za sasa, na kupata uwakilishi unaowajibika zaidi na wenye uwazi zaidi.

“Wengi wa wanachama wa Umoja wa Mataifa wanataka kuwepo marekebisho ya kina ya Baraza la Usalama. Marekebisho hayo yataendeleza kanuni za haki na usawa wa uwakilishi kijiografia, hususan kwa kuzingatia Afrika, bara ambalo bado halina uwakilishi kwenye uanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama, huku wanachama wake kwenye Umoja wa Mataifa wakizidi robo ya wanachama wote, na kuwa chanzo cha zaidi ya asilimia sabini ya ajenda yake.”