Bi Ameerah Haqm azuru jimbo la Unity Sudan Kusini

8 Novemba 2013

Mkuu wa idara inayohusika na maslahi ya walinzi wa amani na wahudumu wa kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Ameerah Haqm amefanya ziara kwenye jimbo la Unity, Sudan Kusini kufanya tathmini ya ujumla ya hali ya mambo. Akiwa katika jimbo hilo, Bi Haqm amekutana na kupewa maelezo na wawakilishi wa serikali kuhusu marekebisho ya katiba, upokonyaji raia silaha na uchaguzi wa mwaka 2015.

Mkutano huo pia umejadili ushirikiano kati ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS na serikali ya jimbo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano na naibu wa Gavana na mawaziri wa jimbo, Bi Haq aliwapongeza viongozi hao wa jimbo kuhusu hatua walizopiga kufikia sasa katika ujenzi wa taifa.

Ametoa wito kwa serikali ijenge taifa thabiti lenye amani na demokrasia, huku akiwapongeza watu wa Sudan Kusini kwa kupata uhuru. Baadaye Bi Haq na Naibu wa Gavana Mabek Lang wamekagua gwaride ya kikosi cha Mongolia kama ishara ya kufurahia kazi yao kwa kuwasaidia watu na mamlaka za Jimbo la Unity.