Mamilioni ya watoto Mashariki ya Kati kupewa chanjo dhidi ya polio

8 Novemba 2013

Zaidi ya watoto milioni 20 katika nchi saba na maeneo ya Mashariki ya Kati wanapewa chanjo dhidi ya polio, kufuatia kulipuka kwa ugonjwa huo wa kupooza nchini Syria. Joshua Mmali na taarifa kamili

(TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

Shirika la Afya Duniani, WHO na lile la Kuhudumia Watoto, UNICEF yanaongoza kampeni hiyo ya utoaji wa chanjo.

Watoto kumi wamepooza kufuatia mkurupuko wa polio katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Syria.

WHO imesema eneo la Mashariki ya Kati halijawa na ugonjwa wa polio kwa takriban mwongo mmoma sasa, lakini katika miezi 12 ilopita, kirusi cha polio kimegunduliwa katika sampuli za uchafu kutoka Misri, Israel, Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza. Sona Bari ni msemaji wa WHO mjini Geneva.

(SAUTI UA SONA)

Nchi husika ni Misri, Iran, Iraq, Jordan, Lebanon, Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza, Syria na Uturuki. Idadi nzima ya watoto ni takriban milioni 22. Hii ni juhudi ya kina ya miezi sita, na kutakuwa na kampeni za mara kwa mara katika kipindi hicho. Kitakuwa kipindi cha juhudi kabambe ili kuongeza kinga mwili ya jamii katika eneo ambalo limekumbwa na mgogoro, na sasa kwa sababu ya idadi kubwa ya watu kuhama, kirusi cha polio kinasambaa kwenye ukanda mzima.”

Bi Bari amesema kamepni hiyo inawalenga watoto milioni 1.6 ndani mwa Syria, ambao watapewa chanjo dhidi ya polio, surua, matumbwitumbwi na rubela.