Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufisadi upigwe vita mitaani hadi vyumba vya mikutano: Ban

Ufisadi upigwe vita mitaani hadi vyumba vya mikutano: Ban

Transparency International, taasisi ya kimataifa inayotetea uwazi imetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameitumia pongezi akisema kupitia ubia wake na taasisi nyingine ukiwemo Umoja huo limesaidia kusongesha vita dhidi ya ufisadi kwenye nchi tajiri na maskini.

Salamu za Ban zimesema ufisadi hauipaswi kugharimu biashara, bali ni uhalifu ambao ni lazima upingwe kuanzia mitaani hadi vyumba vya mikutano. Ametolea mfano mabilioni ya dola yanayopotea kila mwaka kutokana na rushwa kwenye biashara haramu ya silaha na hata binadamu akisema madhara yake ni makubwa kupindukia.

Amesema hatua za kutokomeza ziko bayana akitaja mkataba wa kimataifa dhidi ya rushwa ambao hivi sasa una wanachama 198.

Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa unafanya kazi kwenye baadhi ya maeneo hatari na yasiyo tulivu yanayoweka hatarini kutumbukia kwenye ufisadi na hivyo kunyima haki ya msingi kwa wale wanaohudumiwa. Hata hivyo amesema tayari kuna mifumo ya ndani ya udhibiti na kazi sasa ni kufuatilia na kusimamia ili kuwa mfano wa maadili mema ya utendaji kwa wananchi wanaohudumiwa.