Kimbunga Haiya chapiga Ufilipino UM wasaidia:WMO/OCHA

8 Novemba 2013

Shirika la kimataifa la utabiri wa hali ya hewa WMO linasema kimbunga Haiyan kimepiga Ufilipino na kuelezwa kuwa  ni kikubwa na cha kasi sana, na tayari kimeshasababisha uharibifu mkubwa. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

Kimbunga hicho kinavuma kwa kasi ya kilometa 215 kwa saa na kimeambatana na mvua kubwa. Umoja wa Mataifa unaisaidia serikali ya Ufilipino kutathimini uharibifu uliosababishwa na kimbunga Haiyan, huku Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura ya Umoja wa Mataifa, OCHA ikipeleka timu ya kutathimini majanga nchini humo. Ufilipino ina uwezo mkubwa wa kukabili janga hilo lakini imeomba msaada wa Umoja wa Mataifa. Jens Laerke ni msemaji wa OCHA.

"UM umepeleka timu ya kutathmini majanga ikishirikiana na Umoja wa nchi za kusini Mashariki mwa Asia. Timu hiyo itafanya kazi bila shaka kwa karibu na mamlaka za eneo hilo ili kutathmini mahitaji muhimu kama malazi ya dharura, uratibu, afya, chakula na maji, usafi na mahitaji mengine yanayoweza kujitokeza."

 

Serikali ya Ufilipino imesema kiwango halisi cha athari na uharibifu hakitojulikana hadi kimbunga hicho kitakapomalizika.