Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM-OPCW wathibitisha eneo lililokuwa bado kukaguliwa Syria

UM-OPCW wathibitisha eneo lililokuwa bado kukaguliwa Syria

Hatimaye ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha za kemikali, wameweza kuthibitisha eneo moja kati ya mawili nchini Syria ambayo awali wakaguzi hawakuweza kufika kutokana na sababu za kiusalama.  Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari hatua hiyo ya karibuni huko Aleppo inafanya maeneo yaliyokaguliwa kufikia 22 na bado eneo moja kwa mujibu wa taarifa za maeneo zilizotolewa na Syria na kuthibitishwa na ujumbe huo.

 “Uthibitishaji huo ulifanywa kwa usaidizi wa kamera maalum zilizotumiwa na watendaji wa Syria chini ya mwongozo wa jopo la ukaguzi. Eneo sahihi na wakati ambao picha hizo zilipigwa vimethibitishwa. Eneo hilo limethibitishwa kuwa lilishasambaratishwa na kutelekezwa kwa muda mrefu huku jengo likidhihirisha kukumbwa na uharibifu mkubwa.”

 Wakati huo huo, Farhan amesema ujumbe huo umezindua tovuti yake kwa lengo la kutoa taarifa mbali mbali kuhusu uteketezaji wa mpango wa silaha za kemikali nchini Syria kwa mujibu wa mamlaka iliyopatiwa. Kwa sasa tovuti hiyo yenye anwani http://opcw.unmissions.org itatoa taarifa kwa lugha ya Kiingereza na baadaye lugha ya kiarabu itafuatia