UNEP yakaribisha hatua ya Marekani kuridhia mkataba kuhusu zebaki:

7 Novemba 2013

Marekani imepiga jeki juhudi za kiamataifa za kupunguza gesi chafuzi itokanayo na metali nzito baada ya kuridhia mkataba wa Minamata kuhusu zebaki.

Mkataba huo uliopitishwa tarehe 10 Oktoba mjini Kumamoto Japan na kupewa jina la mji ambao maelfu ya watu walidhurika na sumu ya zebaki katikati ya karne ya 20 sasa umetiwa saini na nchi 93.

Marekani imekuwa ni taifa la kwanza kukamilisha hatua ya mwisho baada ya Kerri-Ann Jones naibu waziri wake wa masuala ya bahari na masuala ya kimataifa ya sayansi na mazingira kuukubali rasmi mkataba huo kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa siku ya Jumatano akisema kuwa mkataba wa minamata ni hatua ya kushughulikia athari za zebaki na kuboresha afya ya jamii.