ITU na INTEL zaingia ubia kuleta mabadiliko kwenye elimu

7 Novemba 2013

Kampuni mashuhuri ya utengenezaji wa chipu za kompyuta, INTEL imeungana na Shirika la kimataifa la mawasiliano, ITU katika kupanua wigo wa matumizi ya teknolojia ili kuleta mabadiliko kwenye sekta ya elimu katika nchi zinazoendelea.

Katibu Mtendaji wa ITU Hamadoun I. Touré amesema ubia huo wakati wa jukwaa la siku nne la teknolojia ya mawasiliano litakalofanyika Bangkok,Thailand utatoa fursa kwa pande mbili hizo kudhihirisha vile ambavyo teknolojia ya habari na mawasiliano inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye elimu.

INTEL itaratibu na kuongoza mijadala kadhaa ikiwemo ule wa kuboresha na kujumuisha mfumo asili wa elimu ili wanafunzi wawe na stadi za karne ya sasa. Halikadhalika kuangalia mbinu za kuwezesha sekta ya umma na binafsi kuchangia miradi ya elimu mtandao.

Touré amesema elimu ni muhimu katika kupanua uwezo wa mtu kufikiri na ndio rasilimali asili inayosambazwa kwa usawa duniani kote.

Jukwaa hilo litaanza tarehe 19 mwezi huu likileta pamoja wadau mbali mbali wakiwemo watunga sera, viongozi wa serikali na sekta binafsi.