Mijeledi na ukatili dhidi ya wanawake ikomeshwe: UM

6 Novemba 2013

Wataalamu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa wametaka kukomeshwa kwa ukatili dhidi ya wanawake hususani ni kuchapwa mijeledi, ikiwamo kwa tuhuma zinazoitwa za kimaadili na kutaka kuheshimwa kwa sheria za kimataifa.

Onyo hili linakuja wakati huu ambapo mwanamke Amira Osman Hamed, ambaye ni mwanaharakati wa haki za wanawake na mhandisi amefikishwa mahakani nchini Sudan kwa tuhuma za kutovaa kimaadili kwa kukataa kufunika kichwa ambapo ikiwa atakutwa na hatia taahukumiwa kwa adhabu ya viboko 40. Kufuatia kusikilizwa kwa kesi hiyo jumatatau bado mwanaharakati huyo anabaki katika utata wa kisheria akisubiri iwapo shitaka linafutwa au kesi kuendelea kusikilizwa.

Akiongea mjini New York Katika mikutano ya vikundi kazi Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, Rashida Manjoo amesema lazima unyanyasaji kwa wanawake kama Amina ukomeshwe akisisitiza kuwa wanawake kama hao, hawapaswi kulazimishwa kuishi katika hofu ya kuchapwa viboko. Amezitaka serkali kukomesha uchapajwi viboko kwa wanawake na wasichana.

Mtaalamu mwingine wa haki za binadamu Frances Raday amesema wanawake ndio ambao kwa asilimia kubwa hupatikana na hatia katika tuhuma ambazo adhabu zake ni kuchapwa mijeledi.